ROHO
MTAKATIFU KATIKA MAOMBI:
Huduma,
Karama na Vipawa
.Na
Shemasi Ismael Salehe
ROHO
MTAKATIFU NA MAOMBI
Mwandishi:
Shemasi
Ismael Salehe


Mawasiliano: simu. +255782317895
+255754480661
+255752513159+255654012268
NB: Hizi ni sura
Nne tu; sura ya Tisa hadi ya Kumi na mbili wasiliana nasi kwaajili ya kupata
kitabu kizima namba hizo hapo juu.
Ili kupata
kitabu hicho itahitaji uchangie kidogo ili kuwezesha kazi hii.
MUNGU
AKUBARIKI!!
ROHO
MTAKATIFU NA MAOMBI
Hatimiliki
Kitabu
hiki ni mali halali ya Shemasi Ismael Salehe. Huruhusiwi kutoa nakala, hadi
upate idhini kutoka kwa wachapishaji au kwa mwandishi wa Kitabu hiki.
©2016
Shemasi Ismael Salehe
SHUKRANI
Namshukuru
Mungu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu kwa kuniwezesha kufanya kazi hii. Pia
nawashukuru wote waliohusika katika kufanikisha uandaaji na uchapishaji wa
kitabu hiki. Kwa kipekee napenda niwashukuru hawa wafuatao:
Familia yangu:
wamekuwa wavumilivu wakati wa mahangaiko ya kuandaa kitabu hiki, pia kwa
ushauri waona maombi.
Mtheologia Johnson P. Pokeaeli: kwa
ukaribu wake kwangu, ushauri, muda na marekebisho ya kazi hii. Pia
amehusikakatika uchangiaji wa mawazo ya kuhakikisha kazi hii inafanikiwa. Ndiye
aliyetengeneza kava la mbele na la nyuma la kitabu hiki.
Mtheologia Yohana E. Kakoa, kwa
kushirikiana na Mtheologia Johnson katika marekebisho ya Kazi hii.
Mtheologia Mary Charamila, Kwa
mchango wake wa mawazo na maombi. Amekuwa mshauri wa karibu kufanikisha kazi
hii.
Jestina Mhando,kwa
ushauri, mapendekezo, maombi na kutia moyo mpaka kukamilika kwa kazi hii.
Profesa Bagandashwa,kwa
kuchangia, kushauri na kutoa marekebisho ya pendekezo la kitabu hiki. Na
kipekee kwa msaada wake wa kifedha kwaajili ya kuchapishwa kwa kitabu hiki.
Daktari, Idahya, kwa
kuchangia kushauri na kutoa marekebisho kwenye pendekezo la kitabu hiki.
Amekuwa mtu wa karibu sana na mwenye utayari wa kunitia moyo wakati wowote na
kunisaidia kimawazo pale nilipohitaji.
Daktari, M.Mbilu, Kwa
kukubali kupitia na kkutoa marekebisho kwenye mapendekezo ya awali ya Kitabu
hiki.
Daktari, E. Ngugi, Kwa
kukubali kupitia na ndiye aliyeandika utangulizi wa kitabu hiki
Mch. Alice Kopwe, kwa
mwaliko wake katika mkutano wa Paska wa wanafunzi wa Sekondari na vyuo,
uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu Korogwe. Kwa mwaliko huo
nilifanikiwa kuandaa somo hili.
Watheologia wenzangu katika
chuo cha SEKOMU. Kwa kunitia moyo na kuchangia baadhi ya
marekebisho katika kitabu hiki.
Mungu
awabariki wote wallioshiriki katika maandalizi na uchapishaji wa Kitabu hiki.
MATAZAMIO YA MWANDISHI WA
ANDIKO HILI KWA MSOMAJI
Naamini
andiko hili litakuwa jibu katika maswali ya watu wengi wanao jiuliza kuhusu
maombi. Wakristo wengi wameshindwa kujua ni kwa nini hawapati majibu ya maombi
yao. Wamefikia hatua ya kukata tamaa na kurudi nyuma katika Imani zao. Wanaomba
lakini hawajibiwi. Wengine wanajiuliza ni kwa nini katika maombi wengine wananena
kwa Lugha (Kuomba katika Roho Mtakatifu) lakini wao hawawezi? Pia kuna maswali
mengi kuhusu hatua za kufuata mtu awapo katika maombi? au Ni faida gani mtu
anayopata anapoomba katika Roho Mtakatifu? au Je! kuna kanuni za kuomba katika
Roho Mtakatifu? au Ni jinsi gani mtu anaweza kujazwa Roho Mtakatifu? Je ni
lazima kila Mkristo awe na ujazo wa Roho Mtakatifu? Na kuna hasara gani za
Mkristo asipokuwa na Roho Mtakatifu? Na
jambo kubwa lililopo katika dunia ya sasa ni Mkristo kukubalika kwa muda
mchache na badae kutokukubalika. Linalopelekea watu wengi kuwa na maswali mengi
kuhusiana na kukubalika au kutokukubalika (Kuwa na kibali) mbele za wanadamu na
mbele za Mungu. Kuna wanao jiuliza; Ni kwanini Mtu (mfanyakazi, au Mtumishi
nk.) anakuwa na kibali kwa muda mfupi tu na baadae kimepotea, mfano anakuwa na
mali badae zinaisha au anakuwa na anakuwa na wafuasi, marafiki wengi lakini
baada ya muda wanamwacha. Yote haya na mengine mengi tutayapata katika
mafundisho haya.
MUNGU AKUBARIKI. AMEN.
YALIYOMO
SURA YA
TISA
UMOJA WA KANISA
Waswahili wanasema “Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu” umoja ni mshikamano,
makubaliano na mapatano ya kundi la watu. Ni mshikamano wa watu wenye nia na
kusudi moja. Ni kufanya kwa pamoja mambo bila kutengana. “Kwa watu wengi umoja
wa Kanisa ni maamuzi ya wakristo kuujenga mwili wa Kristo kwa vipawa
mbalimbali. Hata hivyo tafsiri hii ya umoja wa kanisa, imekuwa ikikosewa na
watu wengine, kwamba haijumuishi uhusiano wa kanisa na Mungu kinagaubaga. Kwa watu kama hawa umoja wa kanisa pia
unajumuisha wakristo na kanisa kwa upande wa Mungu na pamoja na Mungu katika matendo na
dhamira.”(Bagandashwa, 2016)
Mwito wa Mungu
Hili neno mwito linatumika kwa maana ya
kupokea wajibu wa kumtumikia Mungu. Katika wajibu wa kumtumikia Mungu
tunalazimika kuwa na mienendo na tabia zinazompendeza Mungu kama Neno la Mungu
linanyosisitiza kwamba, “mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana,
mkimpendeza kabisa, mkizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi katika
maarifa ya Mungu, mkiwezeshwa kwa uwezo wote, kwa kadiri ya nguvu ya utukufu
wake, mpate kuwa na saburi ya kila namna na uvumilivu pamoja na furaha.” (Kol
1:10_11) Tunahitajika kuzaa matunda ya imani yetu. Tukizaa matunda tutapata
maarifa kutoka kwa Mungu. Mwito wa Mungu unafuatana na uwezo na mamlaka ya
Mungu tukiwa na uvumilivu na kusubiri ahadi za Mungu. Tunapata furaha ya kudumu
wakati tunapomtumikia Mungu. Hebu tuone andiko hili la Biblia linavyosema
kwamba,“Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya
hekima naya ufunuo katika kumjua yeye.Macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue
tumaini la mwito wake jinsi lilvyo na utajiriwa utukufu wa wa urithi wake katika
watakatifu jinsi ulivyo. Na ubora wa uweza wakendani yetu tuaminio jinsi
ulivyo, kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake.” (Efe 1:17_19)
Katika kumfuata na kumtumikia Mungu hakuna
kunia makuu, kufuata Mungu kunaambatana na kuwa na kiasi. Mungu kama apendavyo
amemgawia kila mtu kiasi cha imani “Kwa
hiyo nawasihi, mimi niliyemfungwa katika Bwana, mwenende kama ilivyoustahili
wito wenu mlioitiwa, kwa unyenyekevu na upole na uvumilivu, mkichukuliana na
katika upendo ‘(Efe 4:1-2)
Wito wa kweli unatokana na Mungu Baba wa
utukufu. Aliyeitwa na Mungu amepewa roho ya hekima. Mungu huwapa watumishi wake
roho ya Ufunuo ili waweze kumjua Mungu wa kweli. Ili tufahamu kwa wazi tumaini
letu lazima macho yetu ya ndani yatiwe nuru. Katika kumtumikia Mungu, tunapata
utajiri wa urithi wake. Utendaji wa nguvu za uwezo wake unadhihirisha mamlaka
tunayopata katika wito wa kumtumikia Mungu wetu. Wote wanaomtumikia ni mwili
mmoja katika Roho mmoja. Walioitwa na Mungu wanasaidiana na kusameheana 1The
2:12.
Mtume Paulo anasema, “Maana ufalme wa Mungu
si kula wala kunywa bali ni haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu kwa
kuwa yeye amtumikiaye Kristo katika mambo hayo humpendeza Mungu, tena
hukubaliwa na wanadamu.” (Rum 14:17_18)
Ufalme wa Mungu ni haki amani na furaha
katika Roho Mtakatifu. Katika ushirika wa Roho Mtakatifu ni muhimu kujengana,
Watu wa Mungu ni hekalu la Mungu wakishirikiana ni ushirika wa watakatifu. Roho
Mtakatifu anakaa ndani ya hekalu ambalo ndiyo sisi. Tuthibishe katika Neno
lisemalo, “Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa
Mungu anakaa ndani yenu? Kama mtu akiharibu hekalu la Mungu, Mungu atmharibu
mtu huyo.Kwa maana hekalu la Mungu ni takaatifu, ambalo ndilo ninyi.” (1kor
3:16_17) Tunapokea nguvu, uwezo na mamlaka ya Mungu katika kushirikiana
kumtumikia Mungu. Yesu amejitoa nafsi hata kufa ili atukomboe kutoka kwenye
mauti. Baada ya kukombolewa tumeingizwa kwenye milki na utawala wa Mungu. Hayo
yote ni kwa ajili ya upendo wa Mungu, yatathibitika tukiwa na juhudi katika
kutenda mema. Tunatimiza wajibu wetu wa kumtumikia Mungu duniani na baadaye
tupate kuurithi uzima wa milele.“Bali
ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme taifa takatifu, watu wa milki ya
Mungu, mpate kutangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie
katika nuru yake ya ajabu”(1Pet 2:9).“Ambaye
alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na
kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi katika matendo
mema.” (Tit 2:14)Tumeitwa na Mungu ili atufanye kuwa mzao mteule. Ukuhani
wa kifalme. Taifa takatifu watu wa milki ya Mungu. Tumeitwa tutoke na tutoe
wengine gizani tuingie katika nuru ya kweli yake Yesu Kristo“Ili mwenende kama
ilivyo wajibu wenu kwa Mungu, mweenye kuwaita ninyi ili mwingie katika ufalme
wake na utukufu wake.” (1 The 2:12)
Viungo vya mwili wa Kristo.
“Kwa kuwa kama katika mwili mmoja tuna
viungo vingi, wala viungo vyote havitendi kazi moja. Vivyo hivyo sisi tulio
wengi tu mwili mmoja katika kristo, na viungo kila mmoja kwa mwenzake”(Rum 12: 4 _ 5)
Kutokana na utendaji wa Mungu kama viungo.
Kila mmoja ni tofauti na mwingine. Kwa kutumia vipawa vyetu mbalimbali roho
Mtakatifu huzitenda kazi hizo zote. Roho humgawia kila mmoja kipawa chake kama
apendavyo. Kiungo kimoja kikiumia iwe ni vyote vimeumia. Ndugu yetu wa rohoni
akipatwa na shida iwe ni shida yetu sisi sote. Kiungo kimoja kikitukuzwa viungo
vingine viungane kwa pamoja kufurahi. Siyo Mungu anapomuinua mwenzetu katika
huduma sisi tunachukia. Tufurahi pamoja naye tukimuombea, tukimtia moyo ili
Mungu atuinue na sisi tuliobakia. Bila kutengana tunahitaji kuishindania injili
kwa pamoja. Tupeane misaada tuhakikishe hakuna mwenzetu anayerudi nyuma au
kuanguka dhambini, kwa maana, sisi ni watu washirika lake Yesu Kristo.
Tunamfuata Mungu kwa maana sisi ni watoto wake wapendwa. Tukishirikiana sisi
watoto wake wapendwa. Tukishirikiana na Yesu anatupenda na kututhamini. Mungu
ametutoa dhambini kwa kukubali kumwaga damu yake iwe fidia ya watu wengi ili
waokolewe. Yesu anavyotupenda ni wajibu wetu sisi tulio viungo vya Kristo
kupendana. Sisi ni viungo tukipendana tutalijenga kanisa imara la Kristo
Umoja wa roho
“Basi
pana tofauti za kutenda kazi bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote
katika wote. Lakini kila mmoja hupewa Ufunuo wa Roho katika kufaidiana Lakini
kazi hizi zote huzzitenda Roho huyo mmoja, yeye Yule, akimgawia kila mtu peke
yake kama apendavyo yeye. Na kiungo kimoja kikiumiaviungo vyote huumia nacho,
na kiungo kimoja kikitukuzwa, viungo vyote hufurahi pamoja nacho.” (1Kor
12:6-7, 11, 26)
Tunatofautiana katika kuitenda kazi ya
Mungu vipawa na uwezo wa kila mmoja ni kiungo katika utendaji wa Ki-Mungu.
Tukimtumikia Mungu tunaunganishwa na Roho Mtakatifu azitendaye kazi hizo zote
tukiunganishwa kuwa kitu kimoja. Tunapewa kila mmoja vipawa kama Roho Mtakatifu
apendavyo. Katika kuunganika kwa vipawa hakuna upungufu katika mwili wa Kristo.
Tunahitajika kusimama pamoja katika kumtumikia Mungu. Tunatakiwa kuwa na roho
moja ili kusababishe mafanikio makubwa katika kushindania Injili. Kuwa na moyo
mmoja bila matengano ni mafanikio makubwa katika ulimwengu wa Roho. Mtume Paulo
anaeleza muhtasari umoja wa roho unavyopaswa uwe. Jambo kubwa ni unyenyekevu,
uvumilivu kuchukuliana katika upendo na kuuhifadhi umoja wa Roha katika kifungo
cha imani.
Mambo yafuatayo yanaimarisha umoja wa Roho
·
Bwana mmoja ambaye ni Yesu Kristo.
·
Imani moja.
·
Ubatizo mmoja.
·
Mungu mmoja, muumbaji wa vitu vyote.
·
Kiongozi mmoja.
Hatutahangaika na kitu chochote ikiwa
hatutalaumiana wala kulalamikiana. Tukishikana kwa umoja tutaimarishana pia
hatutampa Ibilisi nafasi ya utawala kwamaana sisi sote ni viungo kwa vipawa
katika mwili wa kristo.
SURA YA
KUMI
HUDUMA
TANO ZA ROHO MTAKATIFU
Mtu
yeyote anapomkubali Yesu awe Bwana na Mwokozi wake amepewa mojawapo.
“Naye
alitoa wengine kuwa mitume na wengine kuwa manabii, na wengine kuwa
wainjilisti, na wengine kuwa wachungaji na walimu” (Efe 4:11).“Lakini tuna
hazina hii katika vyombo vya udongo ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala
si kutoka kwetu. Pande zote twadhikika bali hatusongwi twaona shaka, bali
hatukatitamaa. Twaudhiwa bali hatuachwi, twatupwa chini, bali hatuangamizwi.
Siku zote twachukua katika mwili kuuawa kwake Yesu, ili uzima wa Yesu nao,
udhihirishwe katika Miili yetu.” (2kor.4:7-10). Huduma
hizi zote Mungu kawapa wanadamu wadhaifu. Ila ameweka hazina kubwa kwa nguvu za
Roho Mtakatifu. Zipo changamoto nyingi zinazo kabilli huduma hizi lakini Roho
Mtakatifu anatutia nguvu. Nguvu inayopatikana katika huduma ni ya Mungu
mwenyewe kwa njia ya Roho Mtakatifu. Pia tutambue hakuna huduma isiyo na
makwazo na majaribu bali Roho Mtakatikfu anayaondoa ili watu waamini kuwa Mungu
yupo. Neno la Mungu linatia nguvu kwamba, “kwahiyo
hatulegei, bali japokuwa utu wetu wa Nje unachakaa,lakini utu wetu wa ndani
unafanywa upya siku kwa siku. Maana dhiki yetu nyepesi iliyo ya muda kitambo
tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana.” (2kor.4:16-17).
Mungu anapotupatia huduma mojawapo kati ya hizo tano ni kwa neema sio kwa nguvu
au akili zetu. Kazi ya Mungu tusiifanye kwa ulegevu na woga. Udhaifu wetu wa
kibinadamu usitutishe, huu unachakaa na kuharibika, bali tuangalie mambo ya
Rohoni ili utu wetu wa ndani ufanywe upya. Tuzihesabu dhiki kwamba sio nzito na
hazidumu. Tunapo wahuduumia watu wa Mungu tunangalie utukufu wa Mungu uonekane,
maana yake katika kila tendo la huduma Mungu apewe utukufu. Tunapotumika kwa
uaminifu utukufu wa Mungu unatuzunguka pamoja na wale tunao wahudumia. Zipo
huduma tano ambazo nitazielezea moja moja kama Roho Mtakatifu atakavyo nijalia,
ambazo ni Utume, Unabii, Uinjilisti, Uchungaji na Ualimu.
Utume
Huduma
hii ilikuwa ikiendelea katika historia ya kanisa. Kwa wakati huu huduma hii
inafuatana na ile ya mitume wa kwanza. Huduma hii ni ya kipekee kwasababu
inasimamisha msingi wa mafundisho. Mitume wanaanzisha huduma ya Neno la Mungu
kwa watu ni waenezaji wa hekima ya Mungu. Mitume wanamsukumo wa kipekee wa
kuweka msingi thabiti wa Neno la Mungu .Ni watumishi wenye maono kwa ajili ya
kanisa kwa ujumla. Mitume lazima wawe na Roho Mtakatifu maana kuna magumu
watakayo kumbana nayo katika huduma yao. Mitume hufanya kazi pamoja na hizi
huduma nne zilizobakia. Wao ni wa kiutawala na kiushirika.
Unabii
Manabii
wa Agano la kale walikuwa na kazi ya kutoa unabii pamoja na kutangaza.
Wanapokea unabii kutoka kwa Mungu kuwatangazia wahusika. Nabii hunena akili na
mapenzi ya Mungu kwa ujumbe wa kutabiri, kuongoza hata wakati mwingine
kulisahihisha kanisa. Manabii wawe wakomavu na thabiti katika Neno la Mungu na
aghalabu ni wenye tabia njema. Manabii ni waonaji, watabiri na wanenaji wa
mambo ya Mungu kwa Ufunuo wa maono. Huduma hii ni ya kipekee sana, Mungu ndiye
aliyewapatia. Unabii unatokana na matakwa ya Mungu, wasikilizaji wanaupima kwa
kupitia Neno la Mungu. Mwenye huduma hii anaweza kuonyeshwa mambo mbalimbali
kwa picha au kwa sauti. Wakati mwingine watu wakiwa wanaomba kwa ujumla
unabii unaweza kutokea. Katika kundi la
watu wa Mungu, wapo manabii ambao wana
maono kuhusiana na kundi lakini pia kwa kazi ya Mungu.
Uinjilisti
“Kwa
kadili ilivyozoeleka Mwinjilisti ni Mtumishi ndani ya kanisa ambaye hubeba
dhamana katika kumsaidia Mchungaji wa Usharika.hata hivyo uzoefu unaonyesha
kwamba wapo watu wengine ambao kwa kujitolea kwa wito tu pia hufanya kazi ya
kuwaongoza washarika na wakristo kumwelekea Mungu. Kwa kufanya hivyo watu hawa
huwasaidia wachungaji na watumishi wengine wa kanisa katika kuwaleta kwa Mungu
wao. Kuwapo kwa watu wa aina hii kunaifanya dhana ya Mwinjilisti kuwa pana
zaidi. Ili kuwajumuisha wao na huduma zao” (Bagandashwa, 2016). Kwa maana
hiyo
Mwinjilisti
huduma yake ni kuhubiri injili au habari njema za Yesu Kristo. Anabeba ujumbe
wa Injili kwa ajili ya watu. Mwinjilisti ana mzigo maalumu kwa watu waliopotea.
Mwinjilisti akiwa amebeba mzigo huo hamfichi mtu anamuambia moja kwa moja juu ya
uovu wake. Licha ya watu kuokolewa huduma yao yaweza kuambatana na ishara,
miujiza na maajabu ili kuthibitisha Neno la Mungu. Wanjilisti wanapaswa kuwa
washarika waaminifu kwa kanisa. Kituo cha wanjilisti ni kwa watu waliopotea,
ili watubu waende mbinguni. Kwa ajili ya mzigo kwa waliopotea hatulii hadi watu
wametubu na kumpa Yesu maisha. Wanao wajibu mkubwa wa kuwaeleza wengine kuwa na
mzigo kwa watu waliopotea na kuwaandaa kwa Uinjilisti. Wainjilisti wanamsukumo
wa kuwaelekeza watu wengine kuhusu makosa yao bila kuwaficha, kwa msaada wa
Roho Mtakatifu. Mwinjilisti anakemea, anabomoa dhambi na ngome za shetani.
Anajenga watu kiroho ili wamfahamu Kristo. Mwinjilisti mwenye huduma hii anatoa
mahubiri yenye moto wa Roho Mtakatifu, na watu wanachomwa mioyo na kuamua
kutubu mbele za Mungu.
Uchungaji
Mchungaji
ni cheo cha Mchunga kondoo. Mchungaji ameitwa ili alishe na kutunza kundi la
watu wa Mungu. Mchungaji anahitaji eneo pana la kutolea huduma. Mchungaji ana
uwezo wa kulisha kundi la Mungu kwa Neno la Mungu. “Mchungaji ni mtu aliye
andaliwa maalum kwa kazi hiyo, akawekwa wakfu na akaajikriwa kuitenda kazi
hiyo” (Bagandashwa 2016).
Mtu
mwenye huduma hii ana msukumo toka ndani wa kushauri, kupatanisha,kukusanya na
kulinda kundi lililopo lisitawanyike. Anafahamu kuwa kundi likitawanyika
ataulizwa. Lazima kubeba gharama zinazojitokeza kwa ajili ya kundi la watu wa
Mungu. Mchungaji ni mtu ambaye hatakiwi kuwa na lawana. Ifahamike kuwa wapo
wachungaji wengine wanaoisaidia, na wengine wanaendelea kuitwa na Mungu. Wenye
huduma hii wawe wamekomaa katika Neno la Mungu kwa njia ya maombi.
“Mtu naatuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa
Kristo na mawakilli wa siri za Mungu. Hapo tena inayohitajiwa katika mawakili,
ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu.” (1kor 4:1-2) wenye huduma hii wanatunza
siri za Mungu. Uaminifu unatakiwa uwe
sehemu ya maisha yao. Na watu watambue kabisa kwamba huyu ni mtunzaji wa
siri za Mungu na za watu wa Mungu. Ni jambo muhimu sana kwa mtumishi mwenye
huduma hii kuwa mwaminifu kwa Mungu na kundi analolichunga. Tuyaone maandiko
haya yanavyosema kwamba; “Kwasababu hiyo,
kwakuwa tunahuduma hii, kwa jinsi tulivyopata rehema, hatulegei. Lakini
tumekataa mambo ya aibu yaliyositirika wala hatuenendi kwa hila, wala
kulichanganya Neno la Mungu na uongo, bali kwa kuidhihiriisiha iliiyo
kweli twajionyesha kuwa na haki, dhamiri
za watu zikitushuhudia mbele za Mungu”(2kor.4:1-2). Lazima kuwa na uhakika
kwamba Mungu katika Roho Mtakatifu ndiye aliyewaweka Wachungaji katika huduma.
Kwa huruma na rehema Mungu anapenda kuwatumia, wanapaswa wasiwe walegevu katika
kutimiza wajibu wao mbele za Mungu. Ni muhimu kukataa mambo ya aibu kwasababu
yatalifanya Jina la Mungu litukanwe. Uongo unaoletwa na tamaa katika kundi hili
usiwepo ili kuepuka kulichanganya Neno la Mungu na uongo. Kuwa wenye haki kwa
wanao wachunga na mbele za Mungu. Kutenda haki sio jambo la hiyari bali ni
lazima. Dhamiri au nafsi za watu zikifanyiwa haki au udhalimu zinashtaki na
kushuhudia mbele za Mungu. Ni kundi linalotakiwa lifanye kazi ya Mungu kwa
umakini mkubwa.
Yesu
alimwuliza Petro mara tatu Je Simoni wa Yohana wanipenda kuliko hawa? Akajibu
wewe wajua kwamba nakupenda. Yesu akamwambia Petro chunga kondoo zangu. Wajibu
wa huduma ya Kichungaji ni kulisha kundi kwa Neno la Mungu ili liimarike,
liongezeke na kustawi. Kuchunga ni kuhakikisha kundi halisambaratiki na
halipotei bali linaendelea kuwepo.
Hebu
tuone kidogo ushauri wa Mtume Paulo kwa Timotheo akisema, “Uwakumbushe mambo hayo ukiwaonya machoni pa Mungu, wasiwe na
mashindano ya maneno ambayo hayana faida, bali kuwaharibu wasikiao. Jitahidi
kujionyesha kuwa umekubaliawa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya
kutahayari ukitumia kwa halali Neno la kweli. Jiepushe na maneno ya siyo na
maana, ambayo siyo ya dini, kwakuwa wataendelea zaidi katika maovu.”(2Tim.
2:14-16) Mchungaji akiongozwa na Roho Mtakatifu ataonya na kuwakumbusha
watu wadumu katika kumtegemea na kumtumaini Mungu. Wapo watu wanaopenda
mashindano na mabishano ambayo katika misingi ya Imani hayana faida. Mchungaji
hapaswi kuwa na tabia hiyo bali awasaidie watu hao wasiingie kwenye mshindano.
Mchungaji kwa nguvu za Roho Mtakatifu ni mtenda kazi pamoja na Mungu, hakuna
sababu ya kuona aibu. Maswali na mashindano huzaa magomvi, mwenye huduma ya
kichungaji asiwe mgomvi, bali awe mwanana kwa watu wote. Awezaye kulichukulia
kundi katika mafundisho. Ufuatao ni ushauri wa mtume Paulo kwa watu wenye
huduma hii, “Lihubiri Neno, uwe tayari,
wakati ukufaao na wakati usio kufaa, karipia,kemea na kuonya kwa uvumilivu wote
na mafundisho. Bali wewe uwe na kiasi katika mambo yote, vumilia mabaya, fanya
kazi ya Injili, timiza huduma yako.”(2Tim.4:2,5). Kuna wakati mgumu Roho
Mtakatifu anahimiza kuhubiri na kufundisha Neno la Mungu, hakuna udhuru ni
kwenda kama Roho Mtakatifu anavyosukuma. Ili mradi Roho Mtakatifu amemsukuma
Mchungaji kukaripia, kukemea na kuonya hata wakatae unabaki kuwa ujumbe wa
Mungu. Mchungaji awe na kiasi anayejua kuvumilia mabaya hata kama ameumizwa.
Mchungaji analo sharti la kufanya kazi ya mhubiri wa Injili mpaka kufa.
Ualimu
Huduma
ya mwalimu wa Neno la Mungu ni muhimu kwa ajili ya afya na ustawi wa kundi .
Kanisa lisilo na walimu haliwezi kuimarika wala kukua. Mafundisho ni muhimu
maana tunazama ndani kabisa katika Neno la Mungu. Mwalimu anastawisha kweli
zenye thamani ndani ya maandiko matakatifu. Anahangaika bila kutulia kutafuta
chakula cha kundi liimarike. Mwalimu anapata Ufunuo wa rohoni kwa ajili ya
kufahamu mahitaji ya kundi analolihudumia. Baada ya mwinjilisti kufyeka msitu
na kuwaleta watu kwa kristo walimu wanawafundisha na kuwajenga. Mtu aliyekosa
huduma ya mwalimu kwa kufundishwa ni wepesi wa kuanguka maana katika wokovu
hana mizizi ya kutosha. Katika udongo mzuri anapanda na kunyweshea maji ya
kukuza mbegu. maji yakuzayo ambayo ni Neno la Mungu.
Kwahiyo, Huduma hizi zote tano zinajenga mwili
wa Kristo. Watu waliojaliwa kuwa nazo ni viungo katika mwili wa kristo. Sisi
tulio viungo vya kristo tunapaswa kuhudumiana kwa huduma hizo tano kila mmoja
kwa mwenzake.
SURA YA
KUMI NA MOJA
KARAMA
TISA ZA ROHO MTAKATIFU
Tukitaja
karama tunamaanisha kuwa ni kipawa ambacho Roho Mtakatifu anagawa kama
apendavyo ili utendaji wa kiroho katika mwili wa Kristo ufanyike, Kama Neno la
Mungu linavyosema“Maana mtu mmoja kwa
Roho apewa Neno la hekima na mwengine Neno la Maarifa, apendavyo Roho yeye
Yule. Mwingine imani katika Roho yeye Yule, na mwingine karama za kuponya
katika Roho Yule mmoja na mwingine matendo ya miujiza, na mwingine Unabii, na
mwingine kupambanua Roho, mwingine aina za Lugha na mwingine tafsiri za Lugha.”
(1Kor 12:8-10)
Kila
mmoja anapewa karama kama Roho Mtakatifu apendavyo. Karama ambazo nimefunuliwa
ili tujifunze huzitenda huyo Roho Mtakatifu mmoja peke yake.karama hizo ni hizi
zifuatazo
Neno la
hekima
Karama
hii inahusika katika kuhuisha, kuweka nuru au kugusisha Ufunuo wa Ki-Mungu
ndani ya maisha yetu. Ni mguso maalum ambao Roho Mtakatifu ameutoa. Katika
karama hii Roho Mtakatifu hutoa maono ya ndani na ufahamu wa jinsi ya kuendelea
katika hali fulani.Wakati watu wanahitaji kutenda jambo katika kumtumikia Mungu
wapo watu wanaoshauri ili kundi hilo lisije likaingia kwenye shida. Yesu katika
huduma yake alikuwa na karama hii. Kama tunavyosoma katika Neno la Mungu
“Basi utuambie, waonaje? Ni halali kumpa
kaisari kodi ama sivyo? Lakini Yesu akaufahamu uovu wao akasema, mbona mnanijaribu.
Naowakamletea dinari. Akawaambia ni ya nani sanamu hii, na anuani hii?
Wakamwambia ni kaisari. Akawaambia mlipeni kaisari yaliyo ya kaisari, na Mungu
yaliyo ya Mungu”
(Mt 22:17-22).
Kwa
karama ya Neno la hekima Yesu aligundua mtego wa mashtaka aliotegewa. Hekima
namna hii ni muhimu katika kanisa. Bila kuwa na watu wenye karama ya Neno la
hekima tunaweza kuteswa tukadhani tunateswa kwa ajili ya kristo kumbe tumekosa
hekima toka kwa Mungu.
Vijana
Fulani walikwenda kuhubiri mahali Injili kwa watu wasio wakristo. Walijipanga
bila kuchukua kibali serekalini. Walidhani watafanikiwa. Walisambaratishwa kwa
kupigwa kwa mawe. Walifunguliwa mashtaka wamevunja sheria ya nchi. Walifungwa
wakidhani wanateseka kwaajili ya Kristo kumbe ni ujinga wao. Wangefuata utaratibu
wa kuomba kibali cha Mkutano hayo yasinge wapata. Wahubiri tujitahidi kuwa na
hekima tusidharau taratibu. Karama hii ya Neno la hekima inafanya kazi ndani ya
watu wenye huduma ya unabii na uchungaji.
Neno la
maarifa
Watu
wenye karama hii wanapata Ufunuo wa Ki-Mungu kuhusu kiwango Fulani cha elimu ya
Mungu. Ni mambo muhimu ambayo yanaonyesha kiroho mambo yasiyoonekana kwa macho
ya wanadamu. Ni taarifa ya mambo ya kina ambayo hayawezekani kwa wanadamu.
Uthibitisho wa Neno la maarifa ni mguso wa moja kwa moja au uhuisho wa akili ya
mpokeaji kwa akili ya Mungu ajuaye yote (Yn. 4:18). Ni hali inayoonekana kiroho
lakini kimwili haiwezekani.
Katika
Ufunuo huu hali ya mtu mwenye shida inahamia kwa mtu mwenye Neno la maarifa.
Taabu na maumivu ya mtu mwenye shida yanahamia kwake. Inakuwa hivi maumivu au
matatizo hayo hayakuumizi na yanakuja ghafla. Ukiona hivyo ujue kuna mtu mwenye
hiyo hali. Ndiyo maana wakati mwingine umesikia au utasikia watumishi wakisema
kuna mwenye maumivu kichwani, mgongoni, kifuani nk. hali ile anayoitaja
anaihisi yeye. Huduma zinazoambatana na karama hii ni uinjilisti, ualimu na
utume
Imani
“Na walipokuwa wamekaa wakati mwingi bila
kula chakula, Paulo akasimama katikati yao akasema; wanaume, iliwapasa
kunisikiliza mimi na kutokung’oa nanga huko Krete na kupata madhara haya na
hasara hii. Sasa naawapeni shauri, iweni na moyo mkuu, kwamaana hapana hata
nafsi mmoja miongoni mwenu atakayepotea ila Malekebu tu. Kwa maana usiku huu wa
leo Malaika wa Mungu Yule ambaye mimi ni wake, naye ndiye nimwabuduye,
alisimama karibu nami, akaniambia usiogope, Paulo huna budi kusimama mbele ya
Kaisari; tena, tazama, Mungu amekupa watu wote wanaosafiri pamoja nawe. Basi,
Wanaume changamkeni, kwasababu namwamini Mungu, yakwamba yatakuwa vilevile kama
nilivyoambiwa.”Mdo 27:21-25
Hii ni
karama itolewayo na Roho Mtakatifu kwenda kwa muumini kwa ajili ya hali
zisizowezekana. Inatumika kwa uweza wa Mungu siyo uweza wa Kibinadamu. Imani ni
ule uhakika wa kutimiza majukumu maalimu na kupambana na hali zinazotuzidi uwezo.
Kazi ya karama ya imani ni kutuhifadhi katika hali ya hatari. Unabii unaweza
kutolewa kutokana na lile Mungu analotaka watu walifanye au wasilifanye.
Uponyaji
Karama
za uponyaji ni uwezo wa Ki-Mungu wa kuhudumia uponyaji wa Kimwili na madhaifu.
Tukisema karama za uponyaji ni wingi tukimaanisha kwamba ni uwezo wa uponyaji
wa kimwili, kiroho kiakili hata kisaikolojia. Yesu Kristo anasema,
“Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio
kwa Jina langu watatoa pepo, watasema kwa lugha mpya watashika nyoka, hata
wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa. Wataweka mikono yao juu ya
wagonjwa nao watapata afya” (Mk 16:17-18).Kwa ishara ya kuweka
mikono juu wa wagonjwa wanapokea uzima. Ni nguvu ya Mungu ndiyo inayofanya kazi
siyo ujuzi wa muombaji. Karama hii inafanya kazi pamoja na mitume wainjilisti
na walimu.
Matendo
ya miujiza
Miujiza
ni jambo la Ki-Mungu. Karama hii humhitaji Mungu atende kazi kwa kupitia watu
fulani. Ni kutenda yasiyowezekana kwa akili za wanadamu.“Basi, angalia, mkono wa Bwana u juu yako, nawe utakuwa kipofu,
usilione jua kwa muda, mara kiwi kikamuangukia na giza, akazungukazunguka na
kumtafuta mtu wakumshika mkono na kmwongoza” (Mdo 13:11)Matendo ya miujiza
yanathibitisha Neno la Mungu.
Unabii
Ni
kuruhusiwa kunena chini ya uongozi wa moja kwa moja kutoka kwa Roho Mtakatifu.
Kimsingi waliojaliwa karama hii wanatangaza kwa hali ya kuinuliwa katika Ufunuo
wa kuhuishwa na akili ya Mungu. “Mtu huyu
alikuwa na mabinti wane mabikira, waliokuwa wakitabiri,Basi tulipokuwa tukikaa
huko siku nyingi, Nabii mmoja jina lake Agabo akashuka kutoka Uyahudi.
Alipotufikia aliutwaa mshipi wa Paulo, akajifunga miguu na mikono akasema, Roho
Mtakattifu asema hivi, Ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu watakavyo mfunga mtu
mwenye mshipi huu, nao watamtia katika mikono ya watu wa mataifa.”(Mdo.21:9-11)
Kupambanua
roho
Ni
uwezo wa Ki-Mungu wa kutambua chanzo cha kiroho. Uwezo huo unafuatana na
Nenohisia au tendo ndani ya mtu au kundi la watu au nguvu za giza. Karama hii
inathibitika kwa wote waliojazwa Roho Mtakatifu“Lakini Petro akamwambia, Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe,
kwakuwa umedhania yakuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali. Huna fungu wala
huna sehemu katika jambo hili kwakuwa moyo wako si mnyoofu mbele za Mungu.”(Mdo
8:20-21). Zipo aina nyingi za maroho tusipokuwa na watu wenye uwezo wa
kupambanua tutashindwa na Ibilisi maana atatutegea.
Kunena
kwa lugha
Yapo
Maneno ya Mungu yanayozungumzia kuhusu kunena kwa Lugha kama ifuatavyo: “Petro alivyokuwa akisema maneno hayo Roho
Mtakatifu akawashukia wote walio lisikia lile Neno na wale waliotahiriwa, walioamini,
wakashangaa, watu wote waliokuja na Petro, kwasababu mataifa nao wamemwagiwa
kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha na
kumuadhimisha Mungu.”(Mdo 10:45-46).
Bali yeye ahutubuye asema na watu maneno ya kuwajenga, na kuwafariji na kuwatia
moyo. Yeye anenaye kwa lugha hujijenga nafsi yake bali ahutubuye hulijenga
kanisa.”(1Kor.14:3-4)
Kunena
kwa lugha ni uwezo wa Ki-Mungu wa kuwasiliana na Mungu kwa lugha zaidi ya moja
sliyoizoea. Karama hii inaweza kugusisha lugha za wanadamu au lugha za malaika.
Karama hii hupatikana kwa waamini wote. Hii ni karama pekee inayotusaidia
katika kujijenga kiroho. Ukinena kwa lugha mpya unaongeza chaji za kiroho ndani
yako. Ni msukumo ambao unatoka ndani yetu tuliookoka ili kuteketeza na kuanguasha
ngome na utawala wa ibilisi.
Tafsiri
za lugha
Karama
hii pia ni ya Ki-Mungu. Ufunuo wake umekuja wenyewe. Inahusika katika kutafsiri
tamko linalokuja kwa lugha mpya kwa lugha inayoeleweka kwa watu waliopo. Huku
kutafsiri lugha hakuhusiani na lugha za kawaida bali huja moja kwa moja kutoka
kwa Mungu“Yamkini ziko sauti za namna
nyingi Duniani, wala hakuna moja isiyo namaana. Basi nisipoijua maana ya ile
sauti nitakuwa kama mjinga kwake yeye anenaye: naye anenaye atakuwa mjina
kwangu. Kwasababu hiyo yeye anenaye kwa Lugha na aombe apewe tafsiri. Maana
nikiomba kwa lugha, Roho yangu huomba, lakini akili zangu hazina matunda.”(1Kor
14:10-11, 13-14)Karama hii inaambatana na manabii.
Kwahiyo, Kama wewe ni kiungo katika mwili wa
kristo na unayo kiu ya kupata karama hizi basi Roho Mtakatifu
atatukirimia.Karama hizi zote nilizozifafanua zipo kwa ajili ya kujenga mwili
wa kristo
SURA YA
KUMI NA MBILI
VIPAWA
NANE VYA UTENDAJI KATIKA ROHO MTAKATIFU
Katika
utendaji wa huduma na karama nilizokwisha eleza kila mmoja amepewa vipawa
vyake. Vipawa mtu anazaliwa na kukua akiwa navyo. Tunaweza kuviita ni vipawa
vya umbaji ambavyo havijaboreshwa na Roho Mtakatifu au mafundisho. Watu wengine
hata kama hawajamfahamu Yesu Kristo, kuwa ni Bwana na mwokozi wao, wanayomambo
ambayo wanafanya. Yanatofautiana kati ya mtu na mtu. Tuvione vipawa hivyo
katika Neno la Mungu lisemalo “Basi kwa
kuwa tuna karama zilizo mbali mbali, kwa kadiri ya neema tuliyopewa; ikiwa
Unabii tutoe unabii kwa kadiri ya Imani. Ikiwa huduma yetu; mwenye kufundisha
kwake. Mwenye kuonya katika kuonya kwake; mwenye kurehemu, kwa furaha.”
(Rum.12:6-8). “Uzoefu unaonyesha
kwamba vipawa mtu anazaliwa navyo. Vinajitokeza katika kuendelea kukua.
Wakatianashangaa anafanya akiona ni kawaida, vinaitwa vipawa vya umbaji. Vipo
vipawa ambavyo tunatengenezewa kupitia mafunzo mbalimbali. Hata kwa uwezo wa
Roho Mtakatifu.” (Bagandashwa,2016)Vipawa ambavyo nitavielezea ni kuhudumu,
Kufundisha, kuonya, kukarimu, kusimamia, kurehemu na kuimba.
Kipawa
cha unabii
Kipawa
hiki kinahusika katika kunena chini ya ulaini wa Roho Mtakatifu. Ki-Msingi ni
kipawa cha utendaji chini ya utawala wa Roho Mtakatifu. Kina msukumo wa
kutangaza akili ya Mungu chini ya uvuvio wa kuhuisha. (1Kor 14:13).Kipawa hiki kazi yake kuwatia moyo waliovunjika moyo
na kukatatamaa, waliojeruhiwa na kuumizwa ili wapate nguvu tena.
Kipawa
cha kuhudumu
Kipawa
hiki kinahusu msukumo wa kutumikia ili kukidhi haja iliyopo. Kwa kawaida watu
wenye kipawa hiki ni wasaidizi wenye utayari wa kutumika na kuwajibika. Watu
wenye kipawa hiki wakifanya jambo likifanikiwa wanatosheka, wanardidhika na
kupata amani. Watu hawa wanakuwa ni wa baraka kwa uongozi kwa ajili ya kazi yao
ya kujitolea.
Kipawa
cha kufundisha
Ni
msukumo wa kutafiti na uwezo wa kuwaelezea watu wengine kweli zinazopatikana
katika Neno la Mungu. Ni watu wanaotoa mafunzo ya Neno la Mungu kwa wengine. Ni
wasaidizi katika Shule ya Jumapili, Mikutano ya nyumbani na usafi wa kanisa.
Kutokana na thamani ya kipawa hiki wanaweza kuingia katika huduma ya ualimu “Basi myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzalia
wa Iskanderia, mtu wa Elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika
maandiko. Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwakuwa Roho yake
ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari za Yesu; naye
alijua ubatizo wa Yohana tu.”(Mdo18:24-25).
Apolo alikuwa mtu aliyesoma anayehitaji kujifunza mambo mengi. Alichunguza,
alisoma, alisikiliza na kupekua Neno la Mungu akawa hodari wa maandiko. Naye
alipata nafasi ya kufundisha. Kwa
wengine kipawa hiki kinaanza na kukua polepole hadi kufikia uhodari na ufundi
wa maandiko. Biblia inasema roho yake ilimuaka, maana yake amepata msukumo usio
wa kawaida kufundisha Neno la Mungu kwa usahihi. Wenye kipawa hiki wakifunuliwa
kuwa watu hawajui, watapata msukumo wa kuwafundisha kutokana mahitaji yao.
Kufundisha huku hutokana na msukumo maalumu wa mtu binafsi.
Kipawa
cha kuonya
Kuonya
ni kusihi, kuusia,kutia nguvu,kufariji na kutuliza. Kumtia mtu moyo ni hali
inayotokana na mtu aliyekata tamaa. Mtu mwenye kipawa hiki anauwezo wa
kuwakilisha ushauri kwa kutia moyo na kutoa maonyo na maelekezo sahihi kwa watu
wengine. Mwenye kipawa hiki anaomzigo kwaajili ya kusaidia watu wengine kuonya
ni tendo la kuzaa matunda
Kipawa
cha kukarimu
Mkarimu
ni mtu mwenye kipawa cha utoaji. Anafurahia kuchangia kwa kutoa fedha au mali
kwa ajili ya kazi ya Mungu. Watu wa namna hii wanamsukumo wa kutoa mali zao
bila kujali kupungukiwa. Mkarimu siku zote hatapungukiwa bali atakuwa mtu wa
baraka nyingi kutoka kwa Mungu“Na Yusufu
aliyeitwa na Mitume Barnaba,(maana yake mwana wa faraja), Mlawi, asili yake ni
mtu wa Kipro, alikuwa na shamba, akaliuza, akaileta fedha, akaiweka miguuni mwa
mitume.”(Mdo 4:36-37)
Kipawa
cha kusimamia
Mwenye
kipawa hiki anamsukumo wa pekee wa kuongoza wengine kwa kutimiliza mapenzi ya
Mungu. Wanauwezo wa kushauri na kuongoza wengine katika kustawisha maeneo
mbalimbali ya huduma. Kipawa cha uongozi ni muhimu kwa utendaji wa kazi ya
Mungu. Tusome Neno la Mungu lisemalo “NaMungu ameweka wengine katika Kanisa, wa
kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu miujiza, kasha karama za kuponya
wagonjwa, na masaidiano na maongozi, na aina z lugha.” (1kor 12:28) Katika
mstari huu wa Biblia lengo hasa ni maneno haya “masaidiano na maongozi” ndiyo
yanayoendeana na kipawa cha kusimamia.
Ni budi
kipawa hiki kiwepo katika uongozi wa kanisa la mahali pamoja. (Dhehebu). Ni
muhimu kwa huduma ya kiuchungaji na kitume (Mdo
2:14). Wanakuwa na mzigo ili mambo yasiharibike.
Kipawa
cha kurehemu
Wenye
kipawa cha rehema huonekana kuwa na hisia kali ya huruma kwa wale wanaopata
matatizo au mateso kutokana na kuumizwa. Huruma yao huwaongoza katika matendo
ya huruma, hutia msaada na faraja kwa wahitaji .Chimbuko la rehema ni Mungu
wetu“Bwana amejaa huruma na neema. Haoni
hasira upesi ni mwingi wa fadhili.”(Zab.103:8)“Basi, iweni na huruma, kama Baba
yenu alivyo na huruma. Msihukumu nanyi hamatahukumiwa, msilaumu nanyi
hamtalaumiwa achilieni nanyi mtaachiliwa”(Luka 6:36-37);).Sisi watoto wa Mungu tuliokombolewa tunatakiwa
tuwe na rehema. Tuone uchungu mzito wenzetu wakiteseka. “Heri wenye rehema; maana hao watapata rehema.” (Mt 5:7) kwa mujibu
wa mahubiri ya Yesu anasema wamebarikiwa watu ambao wanawahurumia watu wengine.
Watu wenye kipawa cha kurehemu nao Mungu atawarehemu, sawa sawa na rehema zao.
Hebu tusome pamoja Neno hilimaana hukumu haina huruma yake yeye asiyeona
huruma. Huruma hujitukuza juu ya hukumu.”(Yak.2:1)
Kipawa
cha kuimba
Wenye
kipawa hiki wanamsukumo maalumu wa kumsifu na kumtukuza Mungu. Kutoa sifa kwa
kuimba kunakigusa kiti cha enzi cha Mungu. Wenye kipawa hiki huchangamsha,
huleta uamsho kanisani wakati wote wa makusanyiko. Kuimba ni njia ya kuhubiri
ukuu na Mamlaka ya Mungu.
Kwahiyo, vipawa vyote nane kila mmoja
aliyeokoka amepewa baadhi. Maana yake huwezi kuwa navipawa vyote. Ili tuujenge
ufalme wa Mungu duniani tumuombe Mungu atusaidie kufufua vipawa vilivyokufa.
Hata wewe rafiki yangu ambaye hujampa Yesu maisha, Utakapofanya hivyo na wewe
utakirimiwa vipawa. Tuamke ili tuitende kazi ya
Mungu maadamu ni mchana. “Mwimbieni
Bwana wimbo mpya. Kwa maana ametenda mambo ya ajabu. Mkono wa kuume wake
mwenyewe, mkono wake Mtakatifu umemtendea wokovu. Mfanyieni Bwana shangwe,
dunia yote. Mtumikieni Bwana kwa furaha. Njoni mbele zake kwa kuimba.”
(98:1,99:1). Mfalme Daudi anawahimiza watu wote wamwimbie Bwana.
Tunaimba kwasababu Mungu ametenda mambo ya ajabu. Tunaaowajibu wakuzipaza sauti
zetu mbele za Mungu. Tunapoimba tunatimiza majukumu yetu ya kumtumikia Mungu.
Kuimba ni kuburudisha nafsi zetu na za wengine. Kuimba ni sehemu ya maisha ya
mkristo. Zipo sababu kadhaa zinazotufanya tuimbe wimbo katika kipawa. Kuimba ni
sehemu moiawapo katika Ibada.Mungu anazipenda sifa tunazompazia kwa sauti zetu.
Tunapoimba tunammgusa Mungu. Tunajitahidi kumpendeza Mungu tunapoimba.
Tunammshuuhudia Yesu Kristo kwaajili ya Matendo yake makuu. Kuimba sio hiyari
ni lazima kwa watu wenye kipawa hicho. Nyimbo zinaushushusha uwepo wa Mungu na
kuleta utukufu wa Mungu.
AHSANTE SANA KWA KUSOMA KITABU HIKI.
USIACHE
KUKIOMBEA TAYARI KIPO KINAKAMILIKA TAYARI KWA KUWEKWA DUKANI. Usikose Kupata
kitabu kizima chenye sura zote Kumi na Tatu. Utajifunza Mengi katika hayo yote
utamtukuza Mungu
Mungu Akubariki!!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni